MAISHA CHUO KIKUU

Kuna jambo laniwasha,na kunikera mtima
Ninataka kuwapasha,na munifahamu vyema
Sio jambo la kuzusha,Ni la hakika nasema
Chuo kikuu pasiwe,pa kujifunza muozo

Wazazi ‘mejitahidi,kukulea kwa nidhamu
Nawe ukawaahidi,kuwa utajiheshimu
Ukaongeza zaidi,hutopoteza fahamu
Chuo kikuu pasiwe,pa kujifunza muozo

‘mekuja toka nyumbani,hujui ‘boifurendi’
Leo ‘metokea nini,wavutwa na peremendi
Hata haya hauoni,na darasani huendi
Chuo kikuu pasiwe,pa kujifunza muozo

Nyumbani ulipoketi,vyema ulijisitiri
Leo viminisiketi,watembea kwa fahari
Wavaa nguo za neti, mwili wako wadhihiri
Chuo kikuu pasiwe,pa kujifunza muozo

Hijabu umeiasa, huivai asilani
Unafuata usasa,penseli na vimini
Na haya umeikosa,wajipamba Kama jini
Chuo kikuu pasiwe,pa kujifunza muozo

Ulikuwa huyataki,mambo ya kujipodoa
Leo vilipustiki,tundu nyingi watoboa
Masikio hutosheki,mwatoboa mpaka pua
Chuo kikuu pasiwe,pa kujifunza muozo

Kuswali ‘ mekuwa shida,qibla umekisahau
Unasema huna muda,unaleta na dharau
Moto ni mkali dada,tuzindukeni wadau
Chuo kikuu pasiwe,pa kujifunza muozo

Kwa mipaka tangamana,na wote ajinabii
Jambo la kuhagiana,hilo kwao usitii
Na mikono kupeana,mola wetu haridhii
Chuo kikuu pasiwe,pa kujifunza muozo

‘siwe chombo mwili wako,kila mtu atumie
Ipandishe hadhi yako,nafasi ‘siwapatie
Wakitaka Shari kwako,hao watu wakimbie
Chuo kikuu pasiwe,pa kujifunza muozo

Hebu usiwe rahisi,ukajishusha thamani
Wala ‘siwape nafasi,ukabaki majutoni
Hao wanoitwa fisi,ni hatari si utani
Chuo kikuu pasiwe,pa kujifunza muozo

Mwishoni nimefikia,kwaherini waungwana
Mola ‘kitupa afia,tutazidi kujuzana
Jina mnaulizia? Naona mnanongona
Farwa Shariff nawambia,in shaa Allah tutaonana

Advertisements

UMENIACHIA DONDA

Damu yanitiririka,ja maji ya mchirizi
Na wala sijakatika,ni mawimbi ya simanzi

Umeniachia donda,liso dawa liso tiba

Hainitoki mkononi,wala kwenye langu guu
Yamiminika moyoni,kwa yalonifika makuu
Umeniachia donda,liso dawa liso tiba

Nilikupa wangu moyo,bila shaka bila hofu
Ila roho ulo nayo,umeniachia kovu
Umeniachia donda,liso dawa liso tiba

‘likuona almasi,unangara kama taa
Kumbe mwenzangu ni fisi,waua bila vifaa
Umeniachia donda,liso dawa liso tiba

Roho yako ni nyeusi,huna chembe cha huruma
Una mno ubinafsi,ulotenda yaniuma
Umeniachia donda,liso dawa liso tiba

‘mepata funzo hakika,mapenzi ‘mekuwa sumu
‘mebaki kuhuzunika,kwa sana najihukumu
Umeniachia donda,liso dawa liso tiba

Wanafunzi darasa la nane

Kalamu upande mmoja,na furaha ni wa pili
Tayari kutoa hoja,za wanafunzi jamali
Siku tulioingoja,hakika imewasili
Tumeipata faraja,kwa alama zenu aali

Pongezi zilo mzo mzo,nawapeni wanafunzi
Ningekuwa na uwezo,sikilizeni wapenzi
Ningeliwapa matuzo,japo kuku na vibanzi
Au twende kalisizo,upepo mukabarizi

Mulijifunga kibwebwe, vitabu kakumbatia
Na leo shangwe na mbwembwe,sote tunafurahia
Hivyo mbele musishindwe,kamba mukaachalia
Walishasema wakongwe,elimu ni bora njia

Yote mabonde milima,mulipanda na kushuka
Lengo likawa kusoma, mengine mukayazika
Yote walioyasema,walimu mukayashika
Na leo siku adhwima,matunda yamechipuka

Apaliliae juani,walishasema wahenga
Atalia kivulini,hawakukosa walolonga
Hivyo kuweni makini,huko mbele mukisonga
Walo waovu wendani,mno nao kujichunga

Kupita chumba cha nane,sio mwisho wa safari
Huko mbele mungangane,alama ziwe nzuri
Na mapapa mupigane,ili muvuke bahari
‘kikosolewa ‘sikane,mukaonyesha jeuri

Mwishoni nimewasili,natoa zangu nasaha
Kungia shule  upili,kwa hakika ni furaha
Ila tieni akili,musende fanya mzaha
Mukafanya ujangili,mukaishia na karaha

KUPE KAMGANDA NGOMBE

Nikupe kisa swahibu,kilichomfika ngombe
Yalimkuta masaibu,kikamkata kijembe
Alitafuta majibu,asipate hata chembe
Kupe kamganda ngombe,hakujali zake pembe

Mwenyeji kangia kati,ngombewe kumnusuru
Kwa mno kajizatiti,ili aipate nuru
Karushiwa kibiriti,akapiga kubwa nduru
Kupe kamganda ngombe,hakujali zake pembe

Kupe kainyonya damu,ni nyingi sio kidogo
Damu kaiona tamu,katu hakujali zogo
Kashikilia hatamu,,miaka hadi miongo
Kupe kamganda ngombe,hakujali zake pembe

Mwenyeji kashika tama,hana tena yeye jinsi
Amebaki kulalama,maisha sio rahisi
Imepotea salama,kupe amekuwa nuksi
Kupe kamganda ngombe,hakujali zake pembe

Ngombe amedhoofika,hali yake taabani
Tamaa imekatika,mwenyeji hana amani
Kupe alomakinika,ameleta kisirani
Kupe kamganda ngombe,hakujali zake pembe

MMUMSA ❤

Iwe juu yenu amani,na za mwenyezi rehema
Mabinti na mabanini, natumai mu wazima
Shukurani kwa mannani,kwa kutupa afya njema
Vyote vikiwa ni vyama, mmumsa imeshika namba

Wino mwingi naujaza,kwenye kikalamu changu
Kuyaacha sitoweza,yaliyo moyoni mwangu
Lazima kuyaeleza,muyajuwe wenzi wangu
Vyote vikiwa ni vyama,mmumsa imeshika namba

Udugu alohimiza, mtume wetu hashimu
Vizuri katueleza,si wa peke yake damu
Ni jambo la kupendeza, kushikana isilamu
Vyote vikiwa ni vyama, mmumsa imeshika namba

La msingi letu lengo,ni kudumisha udugu
Na kuyaziba mapengo,bila kuleta vurugu
Kulisimamisha jengo,la dini ya bwana Mungu
Vyote vikiwa ni vyama, mmumsa imeshika namba

Kinatuleta pamoja,chama hiki kilo aula
Kinatuhimiza waja, kumjua wetu mola
Pia twapata faraja,yakitufika madhila
Vyote vikiwa ni vyama, mmumsa imeshika namba

Imetuunganisha kamba,ilo thabiti na ngumu
Hata ‘kitujia simba,au nyoka mwenye sumu
Au wa majini mamba,kuikata ni vigumu
Vyote vikiwa ni vyama, mmumsa imeshika namba

Pamoja twafurahika,furaha iso kifani
Kila tukijumuika,ni faraja si utani
Ni chama cha kusifika,akibariki mannani
Vyote vikiwa ni vyama, mmumsa imeshika namba

Ni moja yetu kabila,kwa mno twajivunia
Kabila isio ila,ya dini isilamia
Zisizo maana mila,zote twazikatalia
Vyote vikiwa ni vyama,mummsa imeshika namba

Twakuomba Mola wetu,mahabba tuzidishie
Udumu udugu wetu,haja zetu tukidhie
Zote tofauti zetu,shimoni tuzifukie
Vyote vikiwa ni vyama, mmumsa imeshika namba

Tuzidi kushikamana,na ndugu tupendaneni
Huruma kuoneana,kinyongo tuondoeni
Na mikono kushikana,kupelekana peponi
Vyote vikiwa ni vyama, mmumsa imeshika namba.

Nimefikia mwishoni,shukurani Kwa rauf
Kalamu naweka chini,naiweka bila hof
Jina langu ikhiwani, ni Farwa binti Shariff
Vyote vikiwa ni vyama, mmumsa imeshika namba

UKIMWI NI JAMBO ZITO

Limetutawala zimwi,tena lenye sumu kali
Munalifahamu zimwi?,linalodhoofisha hali
Si lingine ni ukimwi, ugonjwa usiojali
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Machozi yatiririka,tena njia mbili mbili
Matumbo yanikatika,kwa ilivyokuwa hali
Sina budi kuandika, kuandika yalo kweli
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Ukimwi unasambaa,kama moto wa nyikani
Wanaojiona kung’aa,huingia hatarani
Anasa walozivaa,huwatia mashakani
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Ukimwi gonjwa hatari,linatesa na kuua
Linachoma kama nari,ni nani asiyejua
Kwa hiyo ishi vizuri, maisha yalo murua
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Unajiona kidume,husikii la mwadhini
Leo upo na mwatime, kesho sijui ni nani
Au ni yule salame,ulomkuta shuleni
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Kina binti nanyi pia,tamaa zimewanasa
Maisha mwafurahia,zimewalevya anasa
Mukishaonyeshwa mia,munashindwa kupepesa
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Salimu kakupa gari,Ali kakuita hani
Na yule naye omari,kakupeleka saluni
Huo sio ufahari,unajishusha thamani
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Ukiwa kichwa kigumu, ukimwi upo njiani
Maisha ‘takuwa sumu,yakutoe furahani
Itakupotea hamu,ya kuishi duniani
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Wamezimaliza hela, Kwa madawa kununua
Mwisho wanabaki bila,fikira zawasumbua
Zimewaishia hila,wabaki ‘tungelijua’
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Wengine wetu wendani,walelewa na wazazi
Wamebaki vitandani,hawawezi ‘fanya kazi
Na wazazi masikini,wawalea kwa majonzi
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Mapenzi kabla ya ndoa,tujaribu kuepuka
Ili gonjwa kuondoa,au japo kupunguka
Na wale waliooa,uaminifu kushika
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Jambo moja mufahamu,musilete malumbano
Kuna kusambaza damu, au kudungwa sindano
Kuzijua ni muhimu,njia maarufu mno
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Hivyo tuweni makini,kwa njia nilizotaja
Tusijifanyeni duni,tuzindukeni waja
Tuishini kwa amani,tusiikose faraja
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

Kwa walioathirika,nawapa yangu nasaha
Tamaa ‘sije katika,mukaikosa furaha
Elekeeni kwa rabuka,gonjwa ‘siwape karaha
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga

BABU NA MWANA


MWANA

Shikamoo wangu babu
Kukusalimu wajibu
‘Metuamuru wahabu
Heshima kuwapatia

BABU
Marahaba ya kijana
Habari za tangu jana
‘mefurahi kukuona
Kwako mi najivunia

MWANA
Za tangu  Jana ni njema
Nami pia ni mzima
Sina panaponiuma
Namshukuru jalia

BABU
‘Mefurahi kusikia
Kuna mambo ainia
Nataka kukuambia
Nakusihi zingatia

MWANA
Mimi nimemakinika
Tayari kunufaika
Busara yako hakika
Mimi naiaminia

BABU
Kwanza jambo lilo aula
Muogope wako mola
Usiziache zote swala
Madhambini kajitia

Shikilia sana dini
Iwe thabiti imani
‘kiondoka duniani
Pema upate shukia

Pili hao marafiki
Wengine ni wanafiki
Wakifanya ufasiki
Siwaandame sikia

Na wengine ni wahuni
‘Takutia hasarani
Wakushushe na thamani
Mwishoni ukajutia

Kwa hiyo jiweke mbali
Uyafanye ya halali
Umridhishe jalali
Na wazazi wako pia

Rafiki wa kufuata
Ni yule aso matata
Vitabu huvikamata
Na bidii akatia

Na pia hiyo adabu
Ishikilie shababu
Utaziepuka tabu
Maisha’tafurahia

Nisikilize ghulamu
Wazazi kuwaheshimu
Hilo ni jambo muhimu
Mola kalihimizia

Roho yako iwe Safi
Na laini kama sufi
Mama ‘simwambie uffi
Radhi akakukatia

Na ndugu zako wapende
Usijifanye afande
Kuwapiga kwa makonde
Chuki ukajijengea

Kiunge sana kizazi
Uyajenge na mapenzi
Watu wako uwaenzi
Ni muhimu familia

Haya ukiyafuata
Kweli utametameta
Utangara kama nyota
Katika hini dunia

MWANA
Nimekusikia babu
Hekima yako ajabu
Wala sioni sababu
Maneno kupuuzia

Tafuata hima hima
Yote ulioyasema
Nitashika yalo mema
Maovu kuyakimbia