MAUTI

Bisimilahi karima,mola ulo na huruma.. Shairi hili nasoma,huku kwako naegema.. Nakuomba allahumma,uongoze hunu umma..Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Ndugu Zangu nawambia,mauti Ni ya hakika..Sote yatatufikia,duniani kuondoka..dini yako zingatia, kabla ya siku kufika.. Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Unapofika wakati, maisha yetu hukoma.. Kwani hilo ni sharuti,kulitambua ni vyema..Na sisi hatutoketi,hadi siku ya qiyama.. Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Hivi sasa u mzima,mola wako mshukuru..Kama waweza simama, Mungu usimkufuru..Siku zako zikikoma,upate kuona nuru.. Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Ibada tumesahau,anasa twaziandama.. Mungu tunamdharau,bila ya kurudi nyuma..Twajifanya kusahau,kama kuna na qiyama.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Siku yako ikifika,roho yako itatoka..Hutoongezwa dakika,hata ukalalamika.. Wakati ukishafika, Mungu utamkumbuka.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Izraili akifika,roho yako kuitoa..Wanao watakushika,huku wote wakijua..Siku yako imefika,wote kuwaondokea..Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Watu watakuzunguka, Qurani kukusomea..Hutoweza kutamka,watu wakakusikia..Macho ni yatakutoka,ukiiaga dunia.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Roho ikishakutoka,utalazwa kitandani .. Duniani ‘shaondoka,huna tena thamani..Mali ulioiweka,si yako tena asilani.. Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Watu waanza kulia, kuwaondokea duniani.. Jirani wakisikia,wauliza kuna nini..Habari wataambiwa, umeondoka duniani.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Watu watajumuika,jamaa na majirani..wangoja kukupeleka,kukutana na Maliki.. Lazima kukupeleka,hata kama we hutaki.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Mwili wakishauosha, pamba watakutundika..sanda watakuvalisha,jenezani kukuweka..Mambo yako yamekwisha, utarudi kwa rabuka.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Tulobaki twainama,ni lini yetu sanati..Njia tupate yandama,kuifuata sirati..twamuomba allahumma,jalia wabarakati.. Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Twakuomba ya mannani,mola uso na kifani..Tutilie kaburini,mwangaza ulo na shani..Kaburi liwe bustani,miongoni ya peponi.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Tupe thabiti kauli,tuulizwapo maswali..Utujalie jalali, maswali yawe sahali..Twepushe Moto mkali,utufinike chako kivuli.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Advertisements

WALIMU WETU MAKANDE

Naanza yangu nudhuma,ewe Mola niongoze..Yote nipate yasema, wasojua niwajuze.. Walimu wa sifa njema,heri Mungu awajaze..Heko nawapa pongezi,walimu wetu Makande .

Nimetembea tembea,mabara na visiwani..Ila sijajionea, uzuri uso kifani..Wa walimu wetu hawa, wafunzao kwa makini.. Heko nawapa pongezi walimu wetu Makande.

Ni walimu maridhia,na wa kupendwa na watu..Sifa wamejipatia,kwa uzuri wao utu..Naye mola kawajaalia,mema yasio na kutu..Heko nawapa pongezi,walimu wetu Makande.

Ms Mohammad nikianzia, mwalimu mwenye busara.. Kwenye business kabobea, ywafunza pasi papara.. Tena Mungu namuombea, amuepushe madhila..Heko nawapa pongezi , walimu wetu Makande.

Na Salee naye pia, mwalimu wa kiingereza.. Yeye bidii anatia,Sina budi kumpongeza.. Twampenda nawambia, kimasomo hutuhimiza.. Heko nawapa pongezi ,walimu wetu Makande.

Kwa upande wa kemia,bi Stella aongoza..Na pia kwa fisikia,ni masoni anafunza.. Aidha gografia, kimemia atujuza.. Heko nawapa pongezi,walimu wetu Makande.

Na somo la Kiswahili,pia tunaye mwalimu..Si mwengine Ni meali, mwalimu mwenye nidhamu.. Tunampenda kwa kweli,katu hatuishi hamu.. Heko nawapa pongezi, walimu wetu Makande.

Sikumsahau muteti, mwalimu wa historia..Na somo la hisabati,Ni masoni nawambia.. Wamefanya mikakati,elimu kutupatia.. Heko nawapa pongezi,walimu wetu Makande.

Na pia bwana Makoha, mwalimu mwenye ujuzi..Yeye anafunza lugha,lugha yenye ufunuzi..Tena yenye ufasaha, nao mwingi ufanisi.. Nawambia si mzaha,Yeye Ni mchapakazi .

Nakuomba ya jalali, naomba nami nalia..muhifadhi prinsipali,na shari za kidunia..Ni mwalimu wa kikweli,kufundisha ajulia.. Heko nawapa pongezi,walimu wetu Makande.

Walimu mlosifika, Twawapenda bila shaka.. Twawapenda kwa hakika, shahidi yetu rabuka.. Tena tumefurahika, Makande galzi  kufika.. Miaka minne’mekamilika, twazidi kuwakumbuka.

TUTUNZENI MAZINGIRA

Ndugu zangu waungwana, swali nawaulizeni..Si leo wala si Jana,tatizo hili jamani.. ndilo janga kubwa sana,lililo hapa nchini..Hala hala wananchi,mazingira tutunzeni.

Mazingira yachafuka,sababu Mimi sioni..Ndoo za kumwaga taka,tumeekewa njiani..Sasa vipi twakiuka,zilizoekwa kanuni.. Hala hala wananchi, mazingira tutunzeni.

Wanaoaga dunia,ni idadi kubwa sana..Na wale walobakia, hospitali wamejazana.. Chanzo nikiulizia,watu wengi watakana.. Hala hala wananchi,mazingira tutunzeni.

Ni vyema kujihadhari, wahenga wanatwambia.. Kabla kufika hatari,na kisha tukajutia.. Mazingira Ni fahari,iwapo tutatunzia.. Hala hala wananchi,mazingira tutunzeni.

Na Jambo lingine tena,ni miti kujikatia.. Mvua ‘takosekana,na mimea kutomea..Kisha tutaulizana,bila chanzo kutambua.. Hala hala wananchi,mazingira tutunzeni.

Magonjwa kila aina,yamekithiri nchini..Ni hatari kubwa sana,kuharibu fahamuni..Ni vyema kushikamana,janga hili kuauni.. Hala hala wananchi,mazingira tutunzeni.

Nimefika kikomoni,swali langu nawachia..Suala hili si utani,Ni vyema kuzingatia..Tutieni maanani,tusije tukajutia.. Hala hala wananchi, mazingira tutunzeni.

MAISHA YANGU BILA BABA

Bisimilahi ya mannani, kwa jina lako karima..Mola uso na kifani,natanguliza heshima..Kisha kwa tumwa amini,na ahli zake kirama.. Maisha yangu jamani,bila Baba yaniuma.

Nimeketi na mamangu,ndiye baba ndiye mama..Si mwengine bali wangu,nimpendaye halima.. Kutimiza yalo yangu,mambo yake hujinyima.. Maisha yangu jamani,bila baba yaniuma.

Roho yangu huniuma, wengine kuita Baba.. Nimemzoea mama,sijui kuita baba..Moyo wangu hunithoma,kama nlodungwa mwiba.. Maisha yangu jamani,bila baba huniuma.

Babangu sijamuona,tangu alipoondoka..Hadi sasa Ni kijana,hajui nilipofika..’Menifanya Sina mana,mbeleni ‘tanikumbuka.. Maisha yangu jamani,bila baba yaniuma.

Baba kuwaacha wana,Ni nini kama si dhulma..Tena alosoma sana,ajua ovu na jema..Na wala huruma hana,wana kumuachia mama.. Maisha yangu jamani, bila baba yaniuma.

Metaabika mamangu,hakutaka kutuwacha..Menilea na ndu’ zangu,Khalid shery kimapacha..Na Mimi naapa Mungu,mamangu sitomuacha.. Maisha yangu jamani,bila baba yaniuma.

Baba ndiye kiongozi,tena mwenye majukumu..Sharifu hajamaizi, kwamba kwake ni muhimu..Kutekeleza malezi,na tena kuwa na hamu.. Maisha yangu jamani,bila baba yaniuma.

Metufanya Ni yatima, furaha kutukosesha..Nikikumbuka ya nyuma,yalivyokuwa maisha..alivyoteseka mama,ili kutufurahisha.. Maisha yangu jamani,bila baba yaniuma.
NANI WA KULAUMIWA?

Naanza yangu kauli,kwa marefu na mapana.. Nauliza langu swali, munijibu waungwana..Janga hili si sahali, limetuathiri sana..Swali langu nauliza,nani wa kulamiwa?

Dawa hizi za kulevya, ni hatari nawambia..Usijaribu kuchovya,usije kuja jutia..Marafiki ‘takuponza,iwapo tawasikia..Swali langu narudi,nani wa kulamiwa?

Watu wengi ‘mepotoka, hawana muelekeo..Mashuleni wametoka,si Jana wala si leo..Hela wao wanasaka,za kununua vileo..Sitachoka kuuliza,nani wa kulaumiwa?

Wengine ‘ mekuwa wezi,ati hela watafuta..Za kununua bugizi, ili wapate kuvuta.. Bila Shaka Ni majonzi, kwani mwishowe hujuta..Maswahibu nauliza, nani wa kulaumiwa?

Asosikia la mkuu,wahenga wametwambia..Yeye huvunjika guu,akabaki akilia..Kujidunga mwiba huu,Ni hatari narudia.. Jibu mimi natafuta,nani wa kulaumiw

Nikilaumu wazazi,huenda sijakosea.. Kwani ni yao malezi,wanakosea kulea..wanapofanya uchizi,hawendi kuwakemea..Ni wazazi au nani,watu wa kulaumiwa?

Au tuseme walimu, kwani wao ndio nguzo..Tena ni lao jukumu, kuwapa wana mafunzo.. Vijana vichwa vigumu,wanaweka mapuuzo..Hivyo sidhani walimu,ndio wa kulaumiwa.

Nikisema serikali,ndio wanaochangia..ninashindwa kukubali,moyo unakatalia..lakini mola jalali,ndiye anayejulia.. jamani je serikali,yapasa kulaumiwa?

Dawa hizi ni hatari,shikeni wangu wasia..tamu ya chai sukari,hilo nalihimizia..Jipambeni kwa uzuri,si wa sura ni tabia..Swali langu nauliza,nani wa kulaumiwa?

Ulevi huleta tabu,kwa wana na familia.. Haswa wale mashababu,majutoni huishia..Mukicheza Maswahibu,jelani mutajifia..Mimi nataka kujua,nani wa kulaumiwa?

Wengi ‘mefutwa kazi,eti dawa ndio chanzo..wamejawa na simanzi,dunia ‘mewapa funzo..Ni cha daima kitanzi,na ni mbaya muozo..Na tena nawauliza,nani wa kulaumiwa?

Ulevi huleta ndwele,za aina mbali mbali..Mtu huwa ni muwele,’sifahamu ya awali.. Vidonda humjaa tele,kwenye wote wake mwili..Sichoki kuwauliza, nani wa kulaumiwa?

Jamii ‘mefanya nini,tatizo kuliafiki..Ama wamejimakini,kuwa kwao halifiki..Ni watoto wa jirani, hivyo ndivyo hudhihaki.. Nashindwa kuelewa,nani wa kulaumiwa?

Vijana tuzindukeni,taifa letu kujenga..Dawa hizi tuacheni, mbali nazo kujitenga.. Inshallah mola manani,atatupa ya muanga.. Bila Shaka hatokuwa,mtu wa kulaumiwa.

Kijana jieke mbali,dawa hizi si utani..Aghlabu Ni muhali,kujitoa humo ndani..Hebu tujiwekeni ghali,tuwe na kubwa thamani..Hapo atakosekana mtu wa kulaumiwa.

Nakuomba ya jalali,naomba nami nalia..uwafungue akili, wana wapate tulia..wajikite maskuli,elimu kujipatia..Ili kusipatikane,mtu wa kulaumiwa.

Hapa mwisho nimekoma,sina la kuongezea..Nina mengi ya kusema,mwenyezi yamuelea..Nenda keti huko nyuma,jibu langu nangojea.. Munijibu Maswahibu,nani wa kulaumiwa.

Mashairi ya nudhuma, sita ashra kutimia..Jina langu talisema,Farwa Shariff nawambia..Ni tuombeni salama,na afua na afia..Tuzidi kufikiria,nani wa kulaumiwa?