SWAHABA MCHESHI

Ulimwengu umesheheni watu wenye hulka tofauti tofauti.wapo wacheshi,wachangamfu,wapole,wanyamavu na wengineo wengi ila miongoni mwa wacheshi ulimwenguni naweza sema Nuayman ibn amr Katia fora.

Nuayman alikuwa swahaba aliyetokana na watu wa Banu an Najr katika mji wa Madina.Alifunga pingu za maisha na dada yake Abdurahman ibn Awf na hili Ni thibitisho tosha ya jinsi gani alivyokuwa karibu na mtume swalla llahu alayhi wasallam.Alipigana vita vingi miongoni mwavyo ikiwa Ni
vita vya Badr,uhud na khandaq .

Naam, kama nilivyotangulia kusema kuna watu wenye hulka aina ainati duniani na hizo hulka aghlabu huwa vitambulisho vya watu tofauti tofauti.Nuayman alikuwa maarufu na alitambulika sana kutokana na tabia zake mbili_ unywaji pombe na kufanyia watu utani na kuwachezea shere.Eti nini๐Ÿ˜ณ??? Naam ni Kama ulivyoelewa.Licha ya tabia zake hizo mbili, alikuwa kipenzi cha mtume na mtume alifurahishwa hadi ya kufarihishwa na utani wake.Nuayman alijifunga kibwebwe kujaribu kadri alivyoweza kuacha pombe ila ilimuia vigumu mno.

Alipigwa mboko mara mbili kutokana na unywaji wake wa pombe.Umar alighadhibishwa mno na tabia hiyo na akasema kwa ghamidha kuu, “Mungu akulaani.”mtume alimskia umar na kumkanya papo hapo kwa kumwambia, “la! usifanye hivyo.Hakika anampenda Allah na mtume wake.Dhambi haimueki mja nje ya jamii na huruma iko karibu na wenye kuamini.”Ama kwa hakika, hili linatudhihirishia ya kwamba tusiwabeze ,kuwabeua wala kuwachukia wale wanaofanya madhambi.Mui hui mwema ebo!

Kuna visa vingi vya utani alivyofanya Nuayman na kuwaacha watu katika vicheko vya kuvunja mbavu.Siku moja Nuayman alienda sokoni na kuona vyakula vitamu vya kudondosha mate.Akaona naam! Hii ni fursa adhwimu ya kufanya vitimbi vyake .Aliagizia chakula na kumpelekea mtume Kama zawadi.Mtume alijawa na furaha ghaya na kula chakula hicho pamoja na familia yake kwa bashasha iso mfano.Muuzaji alidai pesa zake na Nuayman akamuelekeza kwa mtume.mtume alishangazwa si haba na kumuuliza Nuayman, ” si ulinipa Kama zawadi?”
“Nilidhani utakipenda chakula hichi ndio maana nikakuletea ila mimi sina hata senti moja mfukoni.” Alisema Nuayman.
Mtume alicheka Sana nao maswahaba wakajiunga katika kucheka huko.Nuayman aliona faida mbili katika hili.Mosi,mtume na familia yake walifurahikia chakula.pili,waislamu waliteremea kwa utani wake.

Si hayo tu.Yapo mengi aliyoyafanya Nuayman yaliochekesha watu na nusra kuvunja mbavu zao.ummu salama aelezea katika hadithi moja kuwa,Abubakar alienda na maswahaba na Nuayman akiwa miongoni katika safari ya kibiashara huko Busra.kila mmoja alipewa kitengo chake Cha kazi na kitengo Cha kuganyiza chakula kikamuangukia suwaybit ibn Harmalah.An-Nuayman alihisi njaa na kumsihi suwaybit ampe chakula.suwaybit akamwambia, ” sikupi chakula mpaka Abubakar anipe ruhusa.”
” Wajua ntakufanyia nini?” Nuayman aliendelea kumuonya ila Nuayman alitia maskio nta na kukataa kuskia la mwadhini wala la mteka maji mskitini.

Nuayman aliamua kumfundisha adabu suwaybit ๐Ÿ˜‚.Alienda guu mosi guu pili hadi katika kundi la waarabu na kuwaambia, “je munataka mtumwa mwenye nguvu,shababu na aliyejengeka kisawa sawa?”
“Ndio” waliitikia waarabu.
“Ila ana ulimi mwepesi na mtakapomchukua atakataa na kusema kuwa yeye ni huru ila musimsikize abaadan kataan!”
Wakakubaliana, waarabu wakalipa ‘qalais’ kumi na kumchukua suwaybit.suwaybit alipiga ukwenzi huku akisema yeye ni mtu huru lakini wapi,waarabu walimbeba hobela hobela na kwenda naye.

Abubakar alipata habari na kuja mbio.Akawaelezea wanunuzi kuwa suwaybit ni mtu huru na kuregeshewa pesa zao.Abubakar, suwaybit na Nuayman walicheka sana baada ya tukio hilo la kuvunja mbavu.Habari zilisambaa Kama mto wa nyika na kufika Madina.Mtume na maswahaba zake aidha walicheka sana walipopata habari hizo.mtume alichukulia vichekesho vyake Kama burudani na ucheshi.Huu ukiwa uthibitisho mwingine kuwa uislamu si dini ngumu kama inavyochukuliwa na wengi.Uislamu ni dini rahisi,ya kupendeza na inayohimiza watu kufurahishana na kueneza tabassam katika nyuso za wengine.

Matukio hayajaisha.kama mbavu zimevunjika,ziunge ujitayarishe kucheka zaidi๐Ÿ˜‚. wakati wa wa uthman in Affan, maswahaba walikuwa msikitini wakamuona Makhramah ibn Nawfal,mzee wa takriban miaka mia na hamsini.Alikuwa kipofu na asiyejiweza.Alitaka kujisaidia na maswahaba wakajaribu kumzuia asijisaidie msikitini.Nuayman alimchukua Kama alivyoagizwa na kumpelekea ili ajisaidie.Alimpeleka wapi!? Mita chache tu na pale alipokuwepo_ ndani ya mskiti bado.watu wakapiga kelele asijisaidie pale naye Nuayman akatimua mbio.mzee alighadhibika Sana na kuuliza aliyemfanyia vile akaambiwa ni Nuayman.
” Nikimpata Nuayman nitamcgaraza kwa bakora yangu,” alisema mzee kwa ghamidha.

Fursa nyingine ilijitokeza kwa Nuayman.Nuayman alimuona uthman akiswali.uthman alikuwa hatingisiki wala hababaishwi na chochote akiwa ndani ya swala.Nuayman alibadilisha sauti na kwenda kumwambia mukramah kuwa Uthman ndiyo Nuayman.Mukramah alimpiga Sana uthman mpka damu ikamchuruzika.watu wakapiga mayowe wakisema ” huyo Ni amir al- mu’minin.”
Watu wakataka kwenda kumleta Nuayman uthman akawakataza.Licha ya majeraha na maumivu aliyoachiwa kwa kipigo kikali, uthman alicheka Sana

Nuayman aliishi hadi Zama za muawiyyah ambapo kulitokea fitna iliyomtia huzuni kubwa na kuanzia wakati huo alipoteza vicheko na utani wake.

Bila shaka, Allah amewaumba viumbe wake na tabia tofauti tofauti.Al muhimu ni kuishi pamoja kwa mapenzi,itifaki,kutambua hulka za wenzetu na kutowadharau au kuwahukumu wale wanaotenda dhambi.Hakika Allah ndiyo al- hakim,Al- ghafur,Al-rahim.

4 thoughts on “SWAHABA MCHESHI

  1. Maa Sha Allah, nice work !

    Liked by 2 people

    1. Shukran ๐Ÿ˜Š

      Liked by 1 person

  2. Mashallah nice work

    Liked by 2 people

    1. ๐Ÿ˜๐Ÿ˜๐Ÿ˜

      Liked by 1 person

Leave a comment