KIPENZI MAMA

Naanza langu shairi,kwa mapozi na madaha.. Nataka kuikariri, niliyonayo furaha..nimepewa na qahari,nakwambia si mzaha..Furaha yenyewe gani? Ni kipenzi wangu mama.

Baada mola karima,na mtume hashimia..Wa kufuata ni mama,nadhani mwanisikia..hivyo tufanyeni hima,mazuri kumtendea..Hata wapande milima, hakuna kama we mama.

Niliyonayo mapenzi, nashindwa kuelezea..Moyo ungekuwa Nazi,basi ningeupasua..Ili kuyaeka wazi, yaliyo kwenye kifua..Uingereza uswazi, hakuna kama we mama.

Wewe Ni fahari yangu,mwanao najivunia..Huburudi moyo wangu,wewe kikufikiria..Huondoka shida zangu,wewe kikuelezea.. Shariani takaungu, hakuna kama we mama.

Hujihisi mi mpweke,mamangu ukiwa mbali..Na natamani niruke,niweko pako mahali..Abadan nisiondoke,niipate mi sahali..Arusha hadi temeke, hakuna kama we mama.

Kikombe tele machozi,mimi hunimiminika..Wala sinayo simanzi,Ila ni kufurahika..kukupata we kipenzi, mama yangu msifika..Lamu na hata kibwezi, hakuna kama we mama.

Hata ‘kijaza kurasa,au kizima kitabu..Maneno sitayakosa,kukusifu we muhibu..Au mbinu za kisasa,zote mi nitajaribu..Canada na ufaransa, hakuna kama we mama.

Cha kukulipa mi Sina,ewe wangu msifika..Ila ahadi nanena,Kuwa utafurahika..Wewe utapaka hina,kwa sana kupumzika..kule India hadi China, hakuna kama we mama.

Na bidii uendazo,ili kunifurahisha..Na kutilia mkazo, mwanao kunisomesha.. Hayo yote si mchezo,taji mi nakuvalisha.. Kampala kalisizo, hakuna kama we mama.

Penzi lingekuwa jani,Basi ningekupa mti..Au Lulu baharini,ningeisaka habibti..Ila kwa yako thamani,nakuombea jannati..Mashariki na kusini, hakuna kama we mama.

Nakuombea mannani,upate umri twawili..Akhera na duniani,uishi kwa njema hali..Na pia kule peponi,uwe na wetu rasuli..Magharibi kaskazini, hakuna kama we mama.

Hapa mwisho nakomea,yanatosha hayo Sasa..Lau nitaendelea,nitazijaza kurasa..Hakika nimetembea,mabara hata Mombasa..Ila sijajionea, mfano kama we mama.

Kama ilivyo desturi,kikomoni nikifika… Mwisho wa langu shairi,jina langu hutamka..Basi ninalikariri,Ni farwatha farshika..Tanga pia Zanzibari, hakuna kama we mama.

Advertisements

2 thoughts on “KIPENZI MAMA

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s