MAUTI

Bisimilahi karima,mola ulo na huruma.. Shairi hili nasoma,huku kwako naegema.. Nakuomba allahumma,uongoze hunu umma..Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Ndugu Zangu nawambia,mauti Ni ya hakika..Sote yatatufikia,duniani kuondoka..dini yako zingatia, kabla ya siku kufika.. Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Unapofika wakati, maisha yetu hukoma.. Kwani hilo ni sharuti,kulitambua ni vyema..Na sisi hatutoketi,hadi siku ya qiyama.. Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Hivi sasa u mzima,mola wako mshukuru..Kama waweza simama, Mungu usimkufuru..Siku zako zikikoma,upate kuona nuru.. Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Ibada tumesahau,anasa twaziandama.. Mungu tunamdharau,bila ya kurudi nyuma..Twajifanya kusahau,kama kuna na qiyama.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Siku yako ikifika,roho yako itatoka..Hutoongezwa dakika,hata ukalalamika.. Wakati ukishafika, Mungu utamkumbuka.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Izraili akifika,roho yako kuitoa..Wanao watakushika,huku wote wakijua..Siku yako imefika,wote kuwaondokea..Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Watu watakuzunguka, Qurani kukusomea..Hutoweza kutamka,watu wakakusikia..Macho ni yatakutoka,ukiiaga dunia.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Roho ikishakutoka,utalazwa kitandani .. Duniani ‘shaondoka,huna tena thamani..Mali ulioiweka,si yako tena asilani.. Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Watu waanza kulia, kuwaondokea duniani.. Jirani wakisikia,wauliza kuna nini..Habari wataambiwa, umeondoka duniani.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Watu watajumuika,jamaa na majirani..wangoja kukupeleka,kukutana na Maliki.. Lazima kukupeleka,hata kama we hutaki.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Mwili wakishauosha, pamba watakutundika..sanda watakuvalisha,jenezani kukuweka..Mambo yako yamekwisha, utarudi kwa rabuka.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Tulobaki twainama,ni lini yetu sanati..Njia tupate yandama,kuifuata sirati..twamuomba allahumma,jalia wabarakati.. Mauti Jambo lazima,kila mtu talionja.

Twakuomba ya mannani,mola uso na kifani..Tutilie kaburini,mwangaza ulo na shani..Kaburi liwe bustani,miongoni ya peponi.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Tupe thabiti kauli,tuulizwapo maswali..Utujalie jalali, maswali yawe sahali..Twepushe Moto mkali,utufinike chako kivuli.. Mauti Jambo lazima, kila mtu talionja.

Advertisements

9 thoughts on “MAUTI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s