NANI WA KULAUMIWA?

Naanza yangu kauli,kwa marefu na mapana.. Nauliza langu swali, munijibu waungwana..Janga hili si sahali, limetuathiri sana..Swali langu nauliza,nani wa kulamiwa?

Dawa hizi za kulevya, ni hatari nawambia..Usijaribu kuchovya,usije kuja jutia..Marafiki ‘takuponza,iwapo tawasikia..Swali langu narudi,nani wa kulamiwa?

Watu wengi ‘mepotoka, hawana muelekeo..Mashuleni wametoka,si Jana wala si leo..Hela wao wanasaka,za kununua vileo..Sitachoka kuuliza,nani wa kulaumiwa?

Wengine ‘ mekuwa wezi,ati hela watafuta..Za kununua bugizi, ili wapate kuvuta.. Bila Shaka Ni majonzi, kwani mwishowe hujuta..Maswahibu nauliza, nani wa kulaumiwa?

Asosikia la mkuu,wahenga wametwambia..Yeye huvunjika guu,akabaki akilia..Kujidunga mwiba huu,Ni hatari narudia.. Jibu mimi natafuta,nani wa kulaumiw

Nikilaumu wazazi,huenda sijakosea.. Kwani ni yao malezi,wanakosea kulea..wanapofanya uchizi,hawendi kuwakemea..Ni wazazi au nani,watu wa kulaumiwa?

Au tuseme walimu, kwani wao ndio nguzo..Tena ni lao jukumu, kuwapa wana mafunzo.. Vijana vichwa vigumu,wanaweka mapuuzo..Hivyo sidhani walimu,ndio wa kulaumiwa.

Nikisema serikali,ndio wanaochangia..ninashindwa kukubali,moyo unakatalia..lakini mola jalali,ndiye anayejulia.. jamani je serikali,yapasa kulaumiwa?

Dawa hizi ni hatari,shikeni wangu wasia..tamu ya chai sukari,hilo nalihimizia..Jipambeni kwa uzuri,si wa sura ni tabia..Swali langu nauliza,nani wa kulaumiwa?

Ulevi huleta tabu,kwa wana na familia.. Haswa wale mashababu,majutoni huishia..Mukicheza Maswahibu,jelani mutajifia..Mimi nataka kujua,nani wa kulaumiwa?

Wengi ‘mefutwa kazi,eti dawa ndio chanzo..wamejawa na simanzi,dunia ‘mewapa funzo..Ni cha daima kitanzi,na ni mbaya muozo..Na tena nawauliza,nani wa kulaumiwa?

Ulevi huleta ndwele,za aina mbali mbali..Mtu huwa ni muwele,’sifahamu ya awali.. Vidonda humjaa tele,kwenye wote wake mwili..Sichoki kuwauliza, nani wa kulaumiwa?

Jamii ‘mefanya nini,tatizo kuliafiki..Ama wamejimakini,kuwa kwao halifiki..Ni watoto wa jirani, hivyo ndivyo hudhihaki.. Nashindwa kuelewa,nani wa kulaumiwa?

Vijana tuzindukeni,taifa letu kujenga..Dawa hizi tuacheni, mbali nazo kujitenga.. Inshallah mola manani,atatupa ya muanga.. Bila Shaka hatokuwa,mtu wa kulaumiwa.

Kijana jieke mbali,dawa hizi si utani..Aghlabu Ni muhali,kujitoa humo ndani..Hebu tujiwekeni ghali,tuwe na kubwa thamani..Hapo atakosekana mtu wa kulaumiwa.

Nakuomba ya jalali,naomba nami nalia..uwafungue akili, wana wapate tulia..wajikite maskuli,elimu kujipatia..Ili kusipatikane,mtu wa kulaumiwa.

Hapa mwisho nimekoma,sina la kuongezea..Nina mengi ya kusema,mwenyezi yamuelea..Nenda keti huko nyuma,jibu langu nangojea.. Munijibu Maswahibu,nani wa kulaumiwa.

Mashairi ya nudhuma, sita ashra kutimia..Jina langu talisema,Farwa Shariff nawambia..Ni tuombeni salama,na afua na afia..Tuzidi kufikiria,nani wa kulaumiwa?

Advertisements

12 thoughts on “NANI WA KULAUMIWA?

  1. Hongera lil sis…mashaallah shairi zuri na lenye ukweli ndani….lakini kwenye ubeti wa saba unapo zungumzia walimu kibwagizo ungeacha swali pia na kusema pia kuwa, “hivyo tuseme walimu ndio wakulaumiwa?”..au ukafanya vyovyote usijibu swali lako nani wakulaumiwa…..good work keep it up

    Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s